28 Aprili 2025 - 22:51
Source: Parstoday
Wafanyakazi 300 wa Google wapinga kuiuzia Israel teknlojia ya AI, inatumika kuua raia Gaza

Wafanyakazi karibu 300 wa Kampuni ya Google nchini Uingereza wamepinga uamuzi wa kampuni hiyo wa kuuza teknolojia ya akili mnemba (AI) kwa makampuni ya usalama yenye uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na kutaka hatua hiyo isitishwe.

Upinzani huo unaonyesha wasiwasi unaoongezeka kuhusu matumizi ya teknolojia ya kisasa katika operesheni za kijeshi na athari zake mbaya kwa binadamu.

Kwa mujibu wa gazeti la Financial Times, hatua hiyo ya mamia ya wafanyakazi wa Google imechukuliwa kufuatia ripoti za uuzaji wa huduma za kompyuta wingu (cloud computing services) na teknolojia ya akili mnemba kwa Wizara ya Vita ya Israel.

Hapo awali, Google iliwafuta kazi wafanyikazi wake 28 kwa kupinga mkataba wa kompyuta wingu na utawala wa Israel unaoendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Wafanyakazi wa DeepMind wameelezea wasiwasi wao kuhusu uwezekano wa kutumiwa teknolojia ya akili mnemba (AI) katika operesheni za kijeshi na wanatoa wito kwa teknolojia hiyo isiuzwe kwa taasisi za ulinzi.

Mwezi Januari mwaka huu, gazeti la Washington Post lilikiri kwamba kampuni ya Kimarekani ya Google imekuwa ikilipatia jeshi la Israel teknolojia ya hali ya juu zaidi ya ujasusi ya akili mnemba (artificial intelligence technologies) tangu wiki za kwanza za mashambulizi ya jeshi la Israel kwenye Ukanda wa Gaza. Gazeti hilo limefichua kwamba ushirikiano kati ya Google na Wizara ya Ulinzi ya Israel ulianza mnamo 2021.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha